Unene na uzito uliopitiliza limekuwa ni tatizo kubwa sana katika jamii yetu kwa sasa. Hili ni tatizo ambalo halipaswi kufumbiwa macho na mtu yeyote mwenye nia njema na afya yake, kwa kuwa athari zake ni kubwa sana kuliko unavyoweza kufikiria. Unene uliopitiliza ni kuzidi kwa mafuta mwilini. Na hii hutokea pale unapoingiza mwilini mwako nishati kubwa kuliko ile inayotakiwa au inayotumiwa na mwili.
Kuongezeka uzito kupita kiasi,au kuongezeka unene kupita kiasi,ni kitendo chenye athari kubwa sana kwa sababu ni mzizi wa magonjwa mengi tena hatarishi sana katika jamii. Madhara ya unene au uzito uliopitiliza zinaonekana wazi kwa watu wanaokabiliwa na matatizo ya presha,kisukari na magonjwa mengine ya moyo. Katika mada hii tutajadili kwa kina madhara yanayoweza kusababishwa na unene au uzito uliopitiliza.
Chanzo Cha Unene Au Uzito Uliopitiliza
Unene uliopitiliza hutokana na kuongezeka sana kwa kalori nyingi mwilini. Kwa kawaida mwili unahitaji nishati (kalori) ili kuuwezesha kufanya shughuli zake za kila siku,na nishati hii hupatikana katika vyakula tunavyokula. Unene au uzito wako hutegemea sana kiasi cha nishati unachokula (kalori katika chakula na vinywaji) na kiasi cha nishati kinachotumiwa na mwili.

-Ukiingiza kiwango kikubwa cha nishati mwilini kuliko kinachotakiwa kutumiwa na mwili,hiki kiwango kilichozidi kitabadilishwa na kufanywa mafuta na kutunzwa mwilini mwako.
-Ukiingiza mwilini kiwango kidogo kuliko kile kinachotakiwa mwilini,mwili wako utabadilisha yale mafuta yaliyotunzwa na kutengeneza nishati ili itumiwe mwilini.
Ili uzito wako uwe katika kiwango kizuri,kiasi cha nishati kinachoingizwa mwilini kinatakiwa kuwa sawa na kiasi cha nishati inayotumiwa na mwili wako. Unene au uzito kupita kiasi hutokana na kuzidi kwa kalori nyingi mwilini kuliko kiwango kinachotakiwa.
Mambo yanayosababisha kalori nyingi kuongezeka mwilini;
Kula vyakula vyenye kalori nyingi- Vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi husababisha kuongezeka kwa kalori nyingi mwilini.
Kula sana kuliko kiwango kinachotakiwa na mwili wako- unapokula sana kuliko kiwango kinachotakiwa na mwili wako,kiwango kinachosalia hubadilishwa na kuwa katika namna ya mafuta na hivyo kutunzwa na mwili na hivyo uzito na unene kuongezeka na kuzidi kulikokawaida kwa haraka.
-Unywaji wa pombe- pombe pia huwa na kiwango kikubwa sana cha kalori hizi na huishia kutunzwa mwilini na kusababisha mafuta ya mwilini mwako kuzidi kiwango kinachatakiwa na kusababisha ongezeko la uzito.
-Kukosa chakula chenye virutubisho- usipokula chakula chenye virutubisho kwa wingi,mwili wako huwa katika hatari ya kudai virutubisho kwa wingi. Hali hii hupelekea kuongeza hamu ya kula kwa wingi na wakati wa kula utakapowadia mtu huyu hula sana jambo linalokusababishia kuongezeka uzito kupita kiasi.
-Kuwa na mzazi mmoja au wote wenye tatizo hili- utafiti unaonesha kuwa vinasaba vya unene hurithiwa kutoka kwa mzazi mmoja na mwingine. Na pia imethibitika kwamba kula sana ama kutokula vizuri kwa mama mjamzito,huweza kubadili DNA ya mtoto na kupelekea athari katika namna ya kutunza na kutumia mafuta mwilini mwake kwa baadaye. Lakini pia baba mwenye tatizo huweza kuliambukiza kwa mtoto kupitia DNA kwenye mbegu.
-Msongo wa mawazo- msongo huathiri ubongo na kupelekea athari katika mfumo wa homoni kama vile cortisol ambayo huratibu ulinganifu wa nishati mwilini na hamu ya njaa. Homoni hii isipofanya kazi kwa kiwango kilichotakiwa mtu hujenga tabia ya kula sana, hali itakayopelekea mafuta mengi kujazwa mwilini na kupelekea kuongezeka unene kupita kiasi.
-Kukosa usingizi wa kutosha- baadhi ya tafiti zimethibitisha uwepo wa uhusiano wa karibu kati ya usingizi na jinsi mwili wako unavyotumia nishati. Na ukosefu wa usingizi huathiri mfumo unaoshughulika na hamu na ulaji wa chakula.
-Matumizi ya madawa- matumizi ya dawa kwa ajili ya kutibu matatizo kadhaa husababisha tatizo la unene. Matumizi ya dawa kama vile steroids na sindano za kuzuia ujauzito husababisha uzito kuongezeka. Lakini pia matumizi ya dawa za kifafa na kisukari pia husababisha tatizo hili kutokea.
-Kuacha kuvuta sigara ghafla- mtu anayevuta sigara na kuacha ghafla,ile hamu na kiu ya sigara huweza kusababisha uzito wake kuongezeka kupita kiasi kwa haraka.
Madhara Ya Unene Au Uzito Uliopitiliza
Miongoni mwa matatizo yenye athari nyingi sana ni tatizo la unene au uzito uliopitiliza. Yapo madhara mengine mengi katika jamii yanayoambatana na uwepo wa tatizo la uzito kuongezeka. Mtu yeyote mwenye tatizo hili huwa katika hatari ya kupata magonjwa mengi na hatarishi kama yafuatayo;
-Magonjwa ya moyo
-Mgandamizo mkubwa wa damu ( high blood pressure)
-Lehemu nyingi mwilini (High cholesterol)
-kisukari
-Matatizo ya mfumo wa upumuaji (Respiratory problems)
-Kuwa na ini lenye mafuta
-Mfadhaiko ( Depression )
-Magonjwa ya maungio ya mifupa-Arthritis
-Kansa
-Asthma
-Kiharusi (Stoke )
-Kukosa usingizi
-Mvurugiko wa siku kwa wanawake
-Hatari ya kufa haraka
-Kutokwa jasho sana
-Upungufu wa vitamini na madini
-Maumivu ya mgongo
-Kukosa uwezo wa kutembea haraka ama umbali mrefu
Jinsi Ya Kudhibiti Tatizo La Unene Au Uzito Kupindukia
Njia zifuatazo zitakusaidia kujiepusha na tatizo la uzito au unene kupindukia:
(i) Kula chakula chenye afya kamili.
Hiki kitaufanya mwili wako kuwa na kalori zinazotakiwa,na kuepusha unene au uzito kupindukia. Chakula hicho ni kama kilivyoainishwa hapa chini;
-Kula chakula aina ya wanga toka kwenye nafaka zisizokobolewa mfano mahindi na ngano
-Epuka chakula chenye mafuta mengi mfano;nyama iliyokaangwa ndani ya mafuta,maziwa yenye mafuta
-Epuka vyakula vyenye sukari kwa wingi kama vile pipi,biskuti,keki na chokoleti
-Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi kwa wingi kama vile nafaka nzima,maharagwe,mchele usiokobolewa (brown rice),matunda na mboga za majani.
- Epuka vyakula vyenye chumvi

(ii) Kuwa na mpango mzuri wa kula
Ili kuepuka tatizo la kuwa na uzito au unene kupindukia,fanya haya kumudu mpango wako mzuri wa chakula:
-Panga ratiba yako ya chakula,fahamu ni wakati gani unakula na unakula nini.
-Kuwa makini na kiasi cha chakula unachokula,usile chakula kingi sana
-Kula milo mitatu, usikose hata mlo mmoja,kukosa mlo mmoja kutakufanya uhisi njaa na kufikiri sana kuhusu chakula na wakati wa kula utakula zaidi ya kawaida jambo ambalo ni hatari.
-Kula tararibu kila wakati ulapo.
- Epuka kula kama umeshiba tayari
(iii) Kuwa makini na vinywaji
Usitumie vinywaji vyenye sukari eti kupoza kiu.Kuna watu wengi hukosea sana pale wanapotumia vinywaji baridi kwa kusudi la kupoza kiu. Hii ni hatari kwa sababu vinywaji hivi vina sukari nyingi na husababisha kalori nyingi kugandamana mwilini na matokeo ya matumizi ya mara kwa mara ni kuongezeka uzito na unene kupita kiasi.Tumia maji kwa wingi kutunza afya yako na kurekebisha uzito wako.
Mambo mengine ya kufanya ili kurekebisha na kuepuka tatizo la uzito mkubwa kupindukia,ni pamoja na kupunguza muda wa kukaa kwenye TV na komputa yako, kupima uzito wako mara kwa mara na kuihimza familia yako kudumisha mfumo bora wa kula ili kuwa na afya njema.
Kufikia hapa ndugu msomaji wangu natumai umejifunza mambo mengi sana kuhusu tatizo la unene au uzito uliopitiliza. Anza sasa kuwa mwangalizi wa afya yako ili kuepuka madhara mengi zaidi. Umeweza kuona kuwa matatizo mengi ya mfumo wa maisha kama vile kisukari,mgandamizo mkubwa wa damu na mengine mengi yote huweza kusababishwa na tatizo la uzito ama unene ulipitiliza. Kuwa mlinzi wa afya yako mwenyewe ili usipoteze thamani ya afya yako.
Je unasumbuliwa na tatizo la unene au uzito uliopitiliza? Wasiliana nasi kupata msaada wa karibu kutatua tatizo lako. Wasiliana nasi kupitia simu 0673 923 959.
Tafadhali wasiliana nasi kupitia Email address maishaniafya@gmail.com ama tupigie kupitia 0673 923 959 ili kupata msaada unaouhitaji. Lakini ukiwa na swali,maoni au ushauri usisite kutuandikia ni furaha yetu kubwa sana kukuhudumia.


