Tatizo la uvimbe kwenye mfuko wa uzazi huwapata wanawake wengi sana. Takribani mwanamke 1 kati ya 5 huweza kupata uvimbe huu katika maisha yao yote. Fibroids ni uvimbe usiosababisha kansa unaotokea kwenye mfuko wa uzazi. Uvimbe huu huwa na ukubwa kama wa harage au njegere na huweza kukua na kuongezeka ukubwa hata kufikia ukubwa wa tikitimaji (melon). Mara nyingi huwapata wanawake wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 50.
Chanzo Cha Uvimbe Kwenye Mfuko Wa Uzazi (Uterine Fibroids)
Chanzo halisi cha tatizo hili la uvimbe,bado hakijajulikana hadi sasa. Lakini mara nyingi limekuwa likihusianishwa na uwepo wa homoni ya oesrogen. Wakati mwanamke anapokuwa na kiwango kikubwa cha oestrogen,uvimbe huu hukua sana. Kwa upande mwingine,kiwango cha homoni ya oestrogen kikipungua uvimbe huu wa mfuko wa uzazi (fibroids) nao hunywea na kupungua.
Wanawake walio na umri kati ya miaka 16 hadi 50 au wanapokuwa wajawazito,ndipo fibroids hukua na kuongezeka kwa kasi,kwa sababu kiwango cha homoni ya oestrogen huwa juu sana. Lakini wanawake waliokoma hedhi,fibroids huanza kunywea kwa sababu kiwango cha homoni ya oestrogen huwa kimeshuka sana.
Aina za Fibroids
.Intramural Fibroids-uvimbe huu hutokea kwenye kuta za mfuko wa uzazi. Ni aina iliyozoeleka na kuenea sana ya fibroids.
.Subserosal Fibroids- Ni uvimbe unaotokea nje ya kuta za mfuko wa uzazi (uterus).
.Submucosal Fibroids- Ni uvimbe unaotokea ndani ya tishu zinazotengeneza kuta za mfuko wa mimba. Uvimbe huu hukua kuelekea uwazi wa mfuko wa uzazi. Wakati mwingine subserosal au submucosal fibroids huweza kushikizwa kwenye mfuko wa mimba na tishu fulani nyembamba,hapa huitwa Pedunculated Fibroids.
Vihatarishi Vya Fibroids
Sambamba na chanzo halisi cha Uvimbe wa fibroids kutojulikana,kuna sababu hatarishi kwa mwanamke yeyote kupata tatizo hili. Sababu hizo ni kama zifuatazo;
-Kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 50
-Kuwa na asili ya Afrika ama visiwa vya Caribean
-Kuwa na ndugu aliyewahi kuwa na ugonjwa huu
-Kutumia nyama nyekundu kwa wingi
-Kunywa pombe kwa wingi
-Kutumia vinywaji vyenye caffeine kwa wingi kama vile soda,cola,majani ya chai n.k
-Kuwa mnene kupita kiasi,maana unene uliopitiliza husababisha kuongezeka kwa homoni ya oestrogen kwa wingi.
Dalili Za Uvimbe Wa Fibroids
Wanawake wengi hushindwa kuhisi dalili za uvimbe huu. Lakini mwanamke 1 kati ya 3 anaweza kupata miongoni mwa dalili zifuatazo;
-Anemia kwa sababu ya kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi
-Maumivu chini ya mgongo
-Kukosa choo
-Maumivu chini ya kitovu hasa kama uvimbe umekuwa mkubwa
-Kukojoa mara kwa mara
-Maumivu wakati wa hedhi,na kutokwa damu nyingi wakati wa hedhi
-Maumivu wakati wa tendo la ndoa
-Maumivu ya miguu
-Kuvimba chini ya kitovu hasa kama uvimbe ni mkubwa
Dalili zingine zaweza kuwa;
-Matatizo wakati wa kujifungua
-Matatizo wakati wa ujauzito
-Ugumba
-Mimba kutoka mara kwa mara
Uchunguzi Wa Fibroids
Utakapokuwa umepata dalili mojawapo au zote kama zilivyooneshwa hapo juu,Utahitajika kufanya uchunguzi. Madaktari watahitali kujiridhisha kama una tatizo la uvimbe kwenye mfuko wa kizazi au ni dalili za tatizo lingine. Miongoni mwa vipimo vinavyotumika kufanya utafiti,kukusaidia kujua kama una tatizo la fibroids ni kama ifuatavyo;
.Ultrasound- Hiki husaidia kuutambua uvimbe huu bila kuathiriwa na uvimbe mwingine wowote uliomo mwilini.
.MRI- Ni kipimo chenye gharama. Lakini hiki husaidia kuonesha kwa usahihi ukubwa wa uvimbe,au kung'amua kama kuna aina zaidi ya moja ya uvimbe mwilini.
.Hysteroscopy- Hiki ni kipimo kidogo cha kutambua ndani ya mfuko wa mimba. Kama itahitajika,wakati fulani kinyama kidogo huchukuliwa toka ndani ya mfuko wa mimba ili kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu maabara.
.Laparoscopy- Hiki ni kipimo kinachohusisha mrija mdogo unaonyumbuka,kinachotumika kupima nje ya mfuko wa uzazi. Kama kutakuwa na uhitaji,kinyama kidogo kitachukuliwa nje ya mfuko na kufanyiwa utafiti. Njia hii huhusisha upasuaji na kuchanwa kwa sehemu fulani ya ngozi yako.
Tiba Ya Fibroids
Fibroids ni tatizo lisilo na madhara kwa asilimia takribani kubwa. Kwa hiyo mwanamke anaweza kuishi na fibroids kwa muda mrefu na asipate madhara. Kama mwanamke ana uwezo wa kutekeleza majukumu yake bila tatizo lolote,na hana haja ya kuzaa tena anaweza kuishi na fibroids bila kuhitaji tiba. Kwa kawaida fibroids huanza kunyauka kabisa mwanamke anapokoma hedhi.
Tiba ya fibroids ikiwa ni lazima kufanyika,mwanamke aweza kupewa dawa ama aweza kufanyiwa upasuaji. Dawa ambazo zimekuwa zikitumiwa kutibu fibroids ni kama zifuatazo;
.Gonadotropin releasing homorne agonist (GnRHA) ambayo hutolewa kama sindano na kuzuia mwili wa mawanamke kutengeneza oestrogen na kusababisha fibroids kukauka.
.Tranexamic acids ni vidonge ambavyo huzuia maumivu na kuzuia mimba pia.
.LINGIUS (Levonorgestrel intrautrine system) hiki ni kifaa kinachoingizwa kwenye uterus.
Tiba kwa njia ya upasuaji huweza kufanyika kwa njia zifuatazo;
Hysteroctomy- hapa uterus huondolewa
Myomectomy-ni upasuaji wa kuondoa fibroids kwenye kuta za uterus
Endometrial ablation-ni upasuaji wa kuondoa ngozi laini ya uterus
UAE (Uterine Artery Embolization)- Ni kuzuia fibroids zisipate damu na hivyo kunyauka. Hii hufanywa kwa fibroids kubwa.
Magnetic-resonance-guided percutaneous laser ablation- Sindano ndogo nyembamba hupenyezwa na kuifikia fibroids. Mionzi humulikwa kupitia waya uliochomekwa kwenye sindano na kuikausha fibroids.
Magnetic-resonance-guided focused utrasound surgery-Kifaa maalum hutumika kugundua mahali fibroid ilipo kisha mawimbi maalum ya sauti huelekezwa kwenye fibroid na kuikausha.
Tumetazama kwa kina tatizo la uvimbe wa Fibroids,ambalo huwasumbua wanawake wengi. Kama una swali,maoni au ushauri kuhusiana na mada hii, tafadhali tujulishe nasi tutashirikiana nawe bila kusita.
Kama una tatizo la fibroids na unahitaji kusaidiwa,wasiliana nasi ili upate msaada. Tuandikie maishaniafya@gmail.com au tupigie 0673 923 959.




