UGONJWA WA MAUNGIO YA MIFUPA - ARTHRITIS

Ugonjwa wa maungio ya mifupa (joint) huwapata watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 50 na kuendelea. Hapa utawasikia akina mama has... thumbnail 1 summary





Ugonjwa wa maungio ya mifupa (joint) huwapata watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 50 na kuendelea. Hapa utawasikia akina mama hasa wenye miili mikubwa wakilalamika sana, mara mifupa inauma,huyu magoti yanauma. Na utawaona wengine wakitembea kwa shida wakiinama huyu hivi huyu vile, mara utasikia wengine joint zangu zinauma hasa pale wanapopanda ngazi au kuchuchumaa. Ama pengine wanapoinuka baada ya kukaa kwa muda mrefu. Tatizo hapa ni nini? Tatizo si kingine bali ni Arthiritis. Ungana nami katika mada hii ili uuelewa ugonjwa huu wa Arthritis.

      Ugonjwa wa Arthritis ni nini?


Arthritis ni ugonjwa unaotokana na namna yoyote ya hitilafu katika maungio ya mifupa ya binadamu ambayo husababisha maumivu au pengine kuvimba kwa sehemu moja ama nyingine ya maungio hayo. Neno Arthritis halilengi ugonjwa mmoja bali ni zaidi ya magonjwa 100 ya jamii moja. Ugonjwa wa Arthritis una tabia ya kusababisha maumivu makali na endelevu katika maeneo ya maungio ya mifupa (joint).


            Chanzo cha Arthritis ni nini?


Arthritis hutokea pale tu kunapokuwa na hitilafu katika maungio ya mifupa. Ili kuuelewa ugonjwa wa Arthritis hebu angalia muundo wa maungio (joint) ya mifupa ya binadamu ulivyo.





        Cartilage:  Ni utando unaofunika mifupa miwili inayokutana pamoja.  Huu huzuia mifupa miwili kusuguana mmoja kwa mwenziwe. Kabla ya mfupa huu kugusa mfupa mwingine katikati kuna cartilage.


Ligament:  Ni kiunganishi cha mifupa. Huunganisha mifupa na mfupa na mfupa na cartilage.

Tendon: Ni kiunganishi cha mifupa na misuli.

Capsule: Hiki ni kitu kinachofunika maungio kikizunguka pande zote. Ndani ya capsule kuna synovial cavity. Ndani ya synovial cavity kuna synovial fluid ambayo huzalishwa na synovial membrane.
Synovial fluid ni ute unaolainisha cartilage na mifupa inayokutana ndani ya capsule ili kuzuia msuguano wa mifupa katika maungio ndani ya capsule.


Sasa Arthritis hutokea pale tu kunapokuwa na hitilafu yoyote kwenye maungio  hayo ya mifupa. Hitilafu hizo huweza kuwa kulika kwa cartilage,upungufu wa synovial fluid pia maambukizi ya vijidudu katika maeneo ya maungio.

Sababu za kutokea arthritis ni; unene au uzito kuzidi,ajali,maambukizi kwenye maeneo ya maungio na  kazi zinazohusisha kukaa au kukunja magoti au mikono kwa muda mrefu.

       Aina za ugonjwa wa maungio ya mifupa-Arthritis


Kama nilivyoeleza hapo juu kuna aina zaidi ya 100 za Arthritis ila hapa tutatazama aina kama nne hivi kwa undani. Karibu ufuatane nami.


Osteoarthritis



Huu ni ugonjwa unaotokea kwenye maungio ya mifupa pale cartiage inaposagika na kupoteza ubora wake. Hii hupelekea mifupa miwili kusagika moja kwa moja na kusababisha maumivu makali katika maungio ya mifupa. Ugonjwa huu huwapata sana wanawake kuliko wanaume hasa wenye miaka 50 na kuendelea japo dalili zake huonekana kuanzia miaka 40. Vijana pia huweza kuupata hasa baada ya ajali au madhara yoyote kwenye maungio.




Ugonjwa huu hushambulia zaidi mikono,magoti,nyonga,shingo na upande wa chini wa mgongo.Huambatana na maumivu makali katika joints, joints hukaza hasa unapoamka asubuhi ama baada ya kukaa kwa muda mrefu,shida katika kutembea na wakati mwingine joints huvimba na kuonekana nyekundu na zenye joto unapozigusa. Huanza taratibu lakini maumivu huongezeka na muda.



Rheumatoid Arthritis




Huu hutokea pale kinga za mwili zinaposhambulia maungio ya mifupa. Kuna wakati kinga za mwili huanza kushambulia eneo fulani la mwili bila sababu na huweza kusababisha matatizo na hii hali huitwa Autoimmune.
Kinga za mwili hushambulia synovial membrane (utando unaofunika bone capsule)  na kupelekea uvimbe na maumivu kwenye joint. Hali hii husababisha mifupa inayozungukwa na synovial  membrane kusagika na cartilage kuharibika na kupoteza ubora wake. Chanzo cha kwa nini autoimmune inatokea bado hakijajulikana.






Ugonjwa huu wa maungio ya mifupa tofauti na osteoarthritis huathiri mwili mzima.Dalili zake ni maumivu ya joint,kukakamaa (kukaza kwa joint) kwa muda wa zaidi ya saa moja,maumivu kifuani wakati wa kupumua,ukavu wa macho na mdomo,macho kuchomana kuwasha,mikono na miguu kuwaka moto,kukosa usingizi,uchovu wa mara kwa mara,mfadhaiko,kupoteza hamu ya kula na upungufu wa damu (anemia).


Ugonjwa huu hupelekea kuathirika kwa viungo vya mwili kama;mapafu na mfumo mzima wa upumuaji, macho,ngozi,mdomo na tezi ya mate,moyo,damu na mishipa ya damu. Unaweza kuona jinsi ulivyo hatari katika jamii.


                   Septic Arthritis



Ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizi yasababishwayo na bacteria ama fangasi na mara nyingi huathiri maeneo ya magoti na nyonga. Maambukizi haya yanaweza kuwapata watu wa rika zote japo watoto wa miaka 3 mara nyingi wameonekana kuwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu pia.


Ugonjwa huu wa maungio ya mifupa husababishwa na;maambukizi ya bacteria popote mwilini,uwepo wa bacteria kwenye damu,magonjwa ya kudumu kama kisukari na sickle cell,matumizi ya dawa zinazopunguza nguvu ya kinga,ajali iliyotokea hivi karibuni,kupandikiza joint na matumizi ya dawa zinazodhoofisha kinga za mwili.


           Juvenile Rheumatoid Arthritis (JRA) 



Madaktari leo pia huuita ugonjwa huu Juvenile Iodiopathic. Ni ugonjwa unaowapata watoto wenye umri chini ya miaka 16. Mara nyingi husababisha homa na upungufu wa damu (anemia). Hupelekea kuathirika kwa mapafu,macho na mfumo wa fahamu.

                              Aina za JRA


Kuna aina tatu za JRA ambazo kwa ufupi tunazieleza sasa;

Pauciarticular JRA 

 Huu huhusisha joint zisizozidi nne hasa kwenye magoti. Ndio aina pekee ya JRA iwapatayo wengi. Takribani nusu (50%)  ya watoto wote wenye JRA wana aina hii ya ugonjwa. Mabinti wenye umri chini ya miaka 8 wengi ndo waathiriwao. Wengi wenye tatizo hili hawana kiwango sawia cha protein katika damu na hudhurika zaidi na matatizo ya macho.

Polyarticular JRA

Huathiri takribani 30% ya wote wenye ugonjwa huu. Huhusisha joint za mikononi na miguuni.


Systemic JRA

Huu huathiri takribani 20% ya watoto wote wenye ugonjwa wa JRA. Mgonjwa hupatwa na homa,kuvimba joint na kuwa na vipele vya pink mwilini. Ugonjwa huu huathiri moyo,Ini na nyongo.  


Kwa sababu ya urefu wa mada hii tutaishia hapa na wakati mwingine tutatazama aina nyingine ya ugonjwa wa ugonjwa wa maungio ya mifupa-ugonjwa wa gout. Asante kwa kukubali kuwa nami katika mada hii,karibu katika mada itakayofuata. Usisite kutoa maoni yako au kuuliza swali lako kuhusiana na mada yetu hii ya leo.

             Je, unasumbuliwa na ugonjwa wa Arthritis? Unaweza kupata tiba bora toka kwetu. Unaweza kuwasiliana nasi sasa
 0673 923 959 au maishaniafya@gmail.com


Usiache kutoa maoni yako,kuuliza swali ulilo nalo au ushauri wako kuhusiana na mada hii. Ni furaha yetu kujumuika nawe katika mfululizo wa mada zetu hizi.





Karibu sana.