UGONJWA WA KISUKARI-NINI CHANZO CHAKE?

Mpendwa msomaji leo tunazungumzia juu ya ugonjwa wa kisukari. Hivi unafahamu kuwa kisukari ni miongoni mwa matatizo hatarishi ... thumbnail 1 summary










Mpendwa msomaji leo tunazungumzia juu ya ugonjwa wa kisukari. Hivi unafahamu kuwa kisukari ni miongoni mwa matatizo hatarishi sana katika jamii yetu leo? Na je, unafahamu kuwa mtu wa  rika yoyote aweza kupata tatizo hili? Lakini pia unafahamu chanzo chake,aina zake,dalili za mtu mwenye kisukari,madhara ya kupata kisukari na tiba ya ugonjwa huu? Ni muhimu sana kwako msomaji wangu kufahamu haya yote. Fuatana nami katika mada hii tutakapojadili mada zote nilizozidokeza hapo juu.

          Chanzo cha Ugonjwa wa kisukari 




Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa magonjwa  yatokanayo na  utendaji kazi wa mwili. Ili mwili wako ufanye kazi zake vyema pasipo shaka yoyote lazima mwili huo upate glucose (sukari) na kuitumia ili kutengeneza nishati. Ni kutokana na nishati hiyo ubongo utafanya kazi yake vizuri,macho, mapafu na viungo vingine mwilini nawe tutakuona unatembea na kufanya majukumu yako kama kawaida. Sambamba na umuhimu huo wa glucose hiyo bado haitakiwi kuzidi,maana ikizidi hiyo ndiyo husababisha ugonjwa wa kisukari. Kwa ufupiugonjwa wa kisukari ni kuzidi kwa sukari (glucose) ndani ya mishipa ya damu.


Mwili wako una tezi iliyo maeneo ya karibu na tumbo lako inayoitwa kongosho. Tezi hii ina seli zinazoitwa Islet ambazo huzalisha homoni inayoitwa Insulini. Insulini ndio homoni yenye kazi ya kuweka msawazo wa glucose (sukari) ndani ya mwili. Homoni hii husaidia kufungua seli za mwili na kuruhusu glucose kufyonzwa na mwili kutoka ndani ya mishipa ya damu kwa ajili ya kuzalisha nishati ili kuleta  utendaji kazi bora  wa mwili. Kama kutakuwa na hitilafu yoyote katika kusharabu sukari kutoka ndani ya mishipa ya damu kuingia ndani ya mishipa ya damu tatizo hili huweza kutokea.Hii hupelekea kiwango kikubwa cha glucose kubaki ndani ya mishipa ya damu na kusababisha tatizo la kisukari.





Chakulakilichoyeyushwa tumboni na kuwa laini (glucose) husharabiwa ndani ya mishipa ya damu. Hiki hutakiwa kubadilishwa na kuleta nishati nishati mwilini. Mchakato huu huratibiwa na insulin inayatolewa na kongosho. Kuna seli pokezi za insulin mwilini (insulin receptor cells) ambazo hupokea insulin na kufunguka ili glucose isharabiwe kwenye mishipa ya damu. Kutopokelewa kwa insulini na seli hizi hata kama imezalishwa kwa kiwango kikubwa sana,huzuia glucose kusharabiwa ndani ya seli za mwili. Hali hii husababisha sukari kuongezeka sana kwenye mishipa ya damu na hatima ya kuongezeka huku ndio ugonjwa wa kisukari.


   Aina za kisukari



Kuna aina tatu za ugonjwa wa kisukari, kama zilivyoelezwa hapa chini;

                                 1.Type 1 Diabetes

Inaitwa kisukari aina ya kwanza. Aina hii ya kisukari hutokea pale kongosho itakaposhindwa kutengeneza insulini kabisa. Hii hupeleakea kiwango chote cha sukari kubaki ndani ya mishipa ya damu, kwa sababu hakuna insulini inayozalishwa na kongosho ili kusaidia kiwango hicho kupunguzwa ndani ya mishipa ya damu. Hali hii hutokana na tatizo linaloitwa  Autoimmune pale kinga za mwili zinaposhambulia seli za mwili kwa bahati mbaya. Na hapa kongosho huharibiwa na kushindwa kufanya kazi yake vyema.


Mgonjwa mwenye ugonjwa huu aweza kuishi kwa kuchomwa sindano za insulini. Kabla ya kugundulika kwa sindano hizi wagonjwa wenye tatizo hili walipoteza maisha sana. Huu mara nyingi huwapata watoto na vijana wenye umri mdogo.

                                              2. Type 2 Diabetes


Aina hii ya ugonjwa hutokea pale kongosho inapozalisha kiwango kidogo sana cha  insulini ama pale mwili unaposhindwa kutumia insulini iliyozalishwa vyema. Kwa kawaida insulini hufungua seli na kuruhusu glucose kupenya na kuingia ndani yake. Kuna wakati insulini yaweza kuzalishwa lakini isipopokelewa na seli (insulin receptors) na kushindwa kufungua seli ili  glucose isharibiwe vyema na seli. Hali hii huitwa Insulin resistance. Chanzo halisi cha insulini resistance hakijulikani japo matumizi ya vyakula venye sukari nyingi huweza kupelekea hali hii. Hali hii hupelekea kiwango kikubwa cha sukari kubakia ndani ya mishipa ya damu bila kusharabiwa ndani ya seli za mwili.


Video hii hapa chini inaeleza kwa ufupi jinsi ugonjwa wa kisukari unavyotokea;





Huwapata watu kuanzia miaka 40 na kuendelea ila kwa waafrika,wachina,wenyeji wa visiwa vya Caribbean na watu wa kusini mwa Asia wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huu kuanzia umri wa miaka 25.  Aina hii ya ugonjwa huweza kuongezeka kutokana na mambo yafuatayo;

-Unene mkubwa kupita kiasi

-Uvutaji wa sigara

-Ulaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha mafuta

-Kutofanya mazoezi ya mwili

-mgandamizo mkubwa wa damu-High blood pressure

-Kunywa pombe kupita kiasi.


 Unaweza ukaona ni aina ya ugonjwa wa kisukari ambayo kwa kiasi kikubwa hutokana na mtindo wa maisha. Hii ni aina ya kisukari inayowakabili watu wengi mno takribani 90% ya watu wote wenye kisukari. Baadhi ya watu wameweza kudhibiti ugonjwa wa kisukari kwa kufanya mazoezi,kupunguza uzito na unene na kufanya vipimo vya mara kwa mara. Usipodhibiti aina hii ya kisukari hukua kila siku na madhara yake pia huongezeka kila siku.

                                            3.Gestational Diabetes


Ni aina ya ugonjwa wa kisukari ambao huwapata akina mama wajawazito. Ugonjwa hu hutokea wakati wa mimba na kutoweka baada ya kujifungua.Huweza kuwa na madhara kwa mmam na mtoto wakati wa kujifungua au baada kama haukugunduluka na kudhibitiwa mapema.  Wanawake wote wanaweza kuathiriwa na ugonjwa huu ila hatari ni kubwa kwa;

-Mwanamke mnene

-Mwanamke aliyewahi kujifungua mtoto mwenye uzito wa 4.5kg au zaidi

-Mwanamke aliyewahi kuwa na tatizo hilo katika mimba iliyopita

-Mwanamke ambaye ni mwafrika au mchina au anatoka kwenye nchi za mashariki ya mbali au kusini mwa asia.

Madhara yake ni makubwa sana ikiwemo mtoto kukua kuliko kawaida,mfuko wa mimba alimo mtoto kujawa na maji kupita kiasi,mama kujifungua kabla ya wakati,mtoto kuzaliwa akiwa na  sukari kidogo jambo litakalopelekea rangi ya ngozi na macho kubadilika na kuwa njano (Jaundice) na pengine hupelekea mama kumpoteza mwanawe.


Je,ungependa kupata msaada kwa tatizo lako la kisukari?Tafadhali wasiliana nasi,upate msaada wa unaohitajika ili kurekebisha afya yako kwa ufanisi wa hali ya juu.

Kufikia hapo mpendwa msomaji wangu tumetazama kwa undani sana jinsi ugonjwa wa kisukari unavyotokea. Nitumie fursa hii kukukaribisha katika  mada itakayofuata tutakapotazama dalili na madhara ya ugonjwa wa kisukari. Karibu uendelee kufuatana nasi.

Kwa maelezo ya kina,msaada ama swali kuhusu mada hii tafadhari wasiliana nasi kupitia maishaniafya@gmail.com au simu 0673 923 959.