Leo mpendwa msomaji,tutatazama tatizo hatarishi na linalosababisha vifo vingi sana,tatizo la kiharusi. Ni watu wachache sana wenye uelewa na tatizo la kiharusi. Kwa kweli ni tatizo hatari,lakini linatibika na kuzuilika kabisa. Tafiti zimebaini kuwa kwa watu wenye ngozi nyeusi hili ni tatizo la 3 kusababisha vifo vingi. Na kwa Wamarekani ni tatizo la 5 kusababisha vifo vingi sana.
Madhara ya kiharusi ni dhahiri. Kwa walio wengi nadhani tumeona watu waliopooza kwa sababu ya tatizo la kiharusi,wengine wanashindwa kuongea au hata kumeza,wanapoteza kumbukumbu na wengine wanapata matatizo ya kihisia na kitabia kabisa. Habari njema ni kwamba tatizo la kiharusi linatibika kwa kutegemea ain ayake na muda mtu alivyodumu akiwa na tatizo. Hebu tulitazame tatizo hili kwa kina sasa.
Kiharusi (Stroke) Ni Nini Hasa?
Kiharusi ni tatizo ambalo hutokea kutokana na damu kushindwa kufika vema kwenye baadhi ya sehemu za ubongo. Hili hutokana na aidha kuziba kwa mshipa ya damu au kupasuka kwa mishipa inayopeleka damu kwenye sehemu fulani ya ubongo. Kuziba au kupasuka kwa mishipa ya damu husababisha seli za ubongo kufa ama kuharibiwa kabisa kutokana na kukosa damu na hivyo kukosa virutubisho na oxygen.
Hitilafu katika mzunguko wa damu kwenye sehemu za ubongo hutokea kutokana na kupungua kipenyo au kuziba kabisa kwa mishipa ya damu. Kuongezeka kwa lehemu nyingi kwenye damu (blood cholestrol) kupita kiasi husababisha tatizo la kupungua kipenyo cha mishipa ya damu (Atherosclerosis). Cholestrol hii huweza kuungana na calcium,fats na vitu vingine na kutengeneza bonge (plaque) linalozuia damu kupita kwenye mishipa ya damu. Plaque huongezeka na wakati mwingine husababisha mshipa wa damu kupasuka.
Chanzo Cha Kiharusi
Ili kuelewa chanzo cha Kiharusi kwanza elewa aina za kiharusi. Kuna aina tatu za kiharusi (stroke). Aina hizo ni kama zifuatavyo:
1.Ischemic Stroke
Hii ni aina iliyozoeleka sana ya kiharusi ikihusisha karibia asilimia 85 ya matatizo yote ya kiharusi. Ni aina ya kiharusi inayotokana na kuziba au kupungua sana kipenyo cha mishipa ya damu ya artery inayopeleka damu kwenye ubongo,na hivyo kupunguza uwingi wa damu kwenye baadhi ya seli za ubongo. Kuziba kwa mishipa mara nyingi husababishwa na kuganda kwa damu na hivyo kutengeneza bonge kubwa (plaque) linalozuia damu kupita. Plaque huweza kutokea kwenye mshipa wa damu kwenye ubongo au mahali pengine na kusukumwa kuelekea kwenye ubongo.
2. Hemorrhagic Stroke
Ni aina ya kiharusi ambayo husababishwa na kupasuka kwa mishipa ya artery na kusababisha damu kuchuruzika kwenye seli za damu. Damu huweza kusambaa kwenye seli za ndani ya ubongo na kuziharibu seli kabisa,au huweza kurukia na kusambaa kwenye uwazi ulio kati ya ubongo na fuvu la kichwa. Sababu kubwa zinazosababisha aina hii ya kiharusi huweza kuwa shinikizo la damu na kudhoofika kwa mishipa ya damu.
3.Transient Ischemic Attack (TIA)
Hii ni aina ya kiharusi ambapo damu hukosa kufika kwenye ubongo kwa muda fulani. Hili likitokea mtu huwa na hali ya kupooza kwa muda mfupi takribani dakika 5. Kama ilivyo kwenye Ischemic damu huzuiwa na kuganda kwa damu kwa muda mfupi. Aina hii ya kiharusi huwa haiachi dalili za muda mrefu kwa sababu kizuizi hiki huwa ni kwa muda mfupi.
Sababu Hatarishi Za Kupata Kiharusi
Sambamba na sababu tajwa hapo juu zinazopelekea kuwepo kwa tatizo la kupooza kwa aina tofauti tofauti kama tulivyoona hapo juu,sababu zifuatazo zaweza kupelekea mtu kuwa katika hatari kubwa ya kupatwa na tatizo la kiharusi. Sababu hizo ni kama zifuatazo:
-Unene uliopitiliza
-Kutofanya mazoezi
-Kunywa kupita kiasi
-Kutumia madawa ya kulevya kama vile cocaine
-Tatizo la high blood pressure
-Kuvuta siagara
-Lehemu nyingi kwenye damu (high blood cholestrol)
-Kisukari
-Kukosa usingizi na oxygen usiku
-Magonjwa ya moyo
-Umri zaidi ya miaka 55
-Kutokea kweny fsmilia yenye historia ya ugonjwa huu
-Asili
-Jisia
Jinsi Ya Kudhibiti Na Kuepuka Kiharusi
Kinga ni bora sana hasa kama tatizo ni hatarishi sana maishani kama ilivyo kwa tatizo la kiharusi.
Ili kujua ni kwa njia gani utaweza kudhibiti na kuepuka kiharusi,lazima uzingatie sababu zinazopelekea litokee. Hatua hizi zitakusaidia kudhibiti madhara ya tatizo zaidi na kuepuka kupata aina nyingine ya kiharusi. Hatua hizi hushabihiana kwa karibu na hatua za kudhibiti na kuepuka magonjwa ya moyo. Kwa ujumla hatua za kufuatwa ili kudhibiti na kuepuka kiharusi ni kama zifuatazo:
.Dhibiti shinikizo lako la damu. Moja ya sababu kubwa zinazochangia kwa haraka mtu kupatwa na tatizo la kiharusi ni shinikizo la juu la damu. Jitahidi kuweka mzunguko wako wa damu katika kiwango cha kawaida. Kupunguza mgandamizo wako wa damu,hukupunguzia hatari ya kupata tatizo hili pia. Soma zaidi jinsi ya kupunguza mgandamizo wa damu kwenye mada tatizo la high blood pressure.
.Punguza ongezeko la lehemu na mafuta mwilini. Kuingiza lehemu (cholestrol) na mafuta kidogo huweza kupunguza utengenezwaji wa mafuta kuganda mwilini (plaque).
Acha kuvuta sigara. Kuvuta sigara huongeza hatari ya kupata kiharusi kwa mvutaji na anaevuta moshi wa mvutaji wa mara kwa mara. Kupunguza uvutaji wa sigara huondoa madhara zaidi ya kiharusi.
.Dhibiti Kisukari. Kisukari huweza kusababisha tatizo la kiharusi.
.Dumisha uzito unaoatakiwa. Uzito wako unapoziti,husababisha vihatarishi vingine vya kiharusi kama vile magonjw aya moyo,kisukari na shinikizo la juu la damu kupamba moto pia.
.Kula matunda na mboga za majani kwa wingi. Kula chakula chenye matunda na mboga kwa wingi huweza kupunguza hatari ya kupata kiharusi kwa kiwango kikubwa.
.Kufanya mazoezi mara kwa mara. Mazoezi huweza kukusaidia kwa namna nyingi kupunguza hatari ya kiharusi. Mazoezi hupunguza shinikizo la damu,hupunguza lehemu isiyofaa mwilini,hupunguza uzito wako,hudhibiti kisukari na hupunguza msongo. Fanya mazoezi angalau dakika 30 kwa wiki au ikiwezekana kila siku.
.Epuka kunywa pombe. Unywaji wa pombe kwa wingi,husababisha tatizo la kiharusi kuongezeka japo inasemekana kuwa kiwango kidogo cha pombe huzuia damu kuganda.
.Epuka matumizi ya madawa ya kulevya. Kutumia dawa za kulevya kama cocaine huongeza hatari ya tatizo la kiharusi. Cocaine hupunguza kipenyo cha mishipa ya damu ya artery na hivyo kuzuia damu kupita kwa ufasaha.
Mpendwa msomaji,tumekuwa na mada ndefu iliyohusu tatizo la kisukari. Kwa kuelewa kwa kina kuhusu tatizo hili kunakusaidia kujikinga na kuliepuka kabisa. Mada itakayofuata tutatazama tatizo la uwingi wa lehemu (cholestrol) mwilini.
Je,una tatizo la stroke na ungependa usaidiwe? Wasiliana nasi kupitia simu 0673 923 959 au maishaniafya@gmail.com.
Kama una swali,maoni ama ushauri kuhusiana na mada hii,usisite tundikie.



