Kansa mwilini hutokea pale seli ndani ya mwili zinapokua na kuongezeka kwa jinsi isiyo ya kawaida. Seli hizi za kansa huendelea kukua na kuongezeka bila sababu kila wakati. Kwa kawaida seli za mwili zina kazi tofauti tofauti na mahususi za kufanya. Seli za mwili huendelea kukua na kuongezeka na kuwa nyingi kila wakati. Zinazochakaa huondolewa na seli mpya huzaliwa. Seli hizi hizi zaweza kukua kwa jinsi isiyo ya kawaida na kuwa kansa. Seli za mwili sehemu yoyote zaweza kuwa kansa. Seli za kansa huongezeka na kuenea sehemu nyingine za mwili.
Kansa ya shingo ya kizazi ni kansa inayotokea kwenye mlango wa kizazi (cervix). Cervix ni upenyo unaotenganisha kati ya mfuko wa uzazi (uterus) na uke wa mwanamke. Kansa ya shingo ya kizazi hutokea pale ambapo seli fulani kwenye kuta za mlango wa kizazi (cervix) zinapokuwa kuliko kawaida. Haitokei mara moja tu seli kuwa kansa,bali seli huanza taratibu kuwa na viashiria vya kansa (pre- cancerous cells). Kwa baadhi ya wanawake viashiria vya kansa huweza kuanza na kupotea,na kwa wengine kuchukua miaka kadhaa kabla seli hizi hazijawa kansa, na kwa wengine seli hizi hukua na kuwa kansa hata ndani ya mwaka mmoja tu. Mwanamke akigundulika mapema kuwa na viashiria vya kansa,anaweza kupata tiba na kupona kansa ya shingo ya kizazi haraka na kwa ufanisi kabisa.
Aina za kansa ya shingo ya kizazi
Kuna aina mbili kuu za kans aya shingo ya kizazi;
Squamous cell carcinoma-Takribani kansa 9 kati ya 10 huwa ni za aina hii. HIzi hutokea kwenye seli za exocervix na kuenea. Mara nyingi huanzia pale exocevix inapokutanan aendocervix.
Adenocarcinomas-Hizi ni kansa zinazotokea kwenye seli zinazotengeneza ute (mucus) za endocervix. Ni aina ya kansa iliyokuwa imeshamiri miaka 20 hadi 30 iliyopita.
Chanzo cha Kansa ya shingo ya kizazi
Sababu kadha wa kadha zaweza kuchangia wewe kupata kansa ya shingo ya kizazi. Sababu ni kama zifuatazo;
Maambukizi ya Human Papilloma Virus (HPV)-Maambukizi ya virus hivi ni chanzo kikuu cha tatizo hili. Kuna aina zaidi ya 100 za virus hivi,lakini sio virus vyote huweza kusababisha aina hii ya kansa. Zaidi ya 70% ya kansa zote za mlango wa kizazi husababishwa na HPV 16 na HPV 18. Virus hivi huenezwa kwa njia ya kujamiiana kati ya mwanamke na mwanamume.
Msongo wa mawazo-wanawake wenye msongo kwa muda mrefu kwao ni vigumu sana kudhibiti HPV. Wanawake wanaotumia madawa na pombe kudhibiti msongo huwa katika hatari ya kutodhibiti virusi vinavyosababisha kansa vya HPV.
Mahusiano na mimba katika umri mdogo-Mwanamke aliyepata mimba katika umri wa miaka 17 au chini ya hapo,huwa katika hatari mara mbili zaidi ya kupata kansa ya shingo ya kizazi kuliko aliyepata mimba katika umri wa miaka 25 au zadi.
Hali ya kiuchumi-tafiti zimebaini kuwa wanawake wengi walio katika mazingira magumu hukumbwa na hili tatizo la kansa ya kizazi. Hii huweza kusababishwa na kukosa virutubisho vya kutosha kuufaa mwili.
Kukosa matunda na mboga kwa wingi-Mwanamke anayetumia matunda na mbogamboga kwa kiwango kidogo sana ana hatari kubwa ya kupata kansa ya mlango wa kizazi.
Uzito uliopitiliza-wanawake wenye uzito mkubwa wana hatari kubwa ya kupata kansa ya Adenocarcinomas.
Kinga Dhaifu-kinga ya mwili huharibu seli za kansa na kuzuia ukuaji wake. Kwa mwanamke mwenye UKIMWI wana hatari kubwa ya kupata kansa hii. Lakini pia mwanamke aneyetumia madawa ya kulevya,aliyefanyiwa upasuaji wa kuondoa au kuongeza kiungo fulani mwilini,kinga yake ni ndogo na ni rahisi kwake kupatwa kansa hii.
Kuvuta sigara-wanawake wanovuta sigara huwa katika hatari mara mbil zaidi ya wale wasiovuta kabisa. Tafiti zimebaini kuwa chembe chembed za nicotine iliyo kwenye sigara hubakia kwenye ute (mucus) wa mlango wa kizazi (cervix),kwa mwanamke anayevuta sigara. Chembe chembe hizi huharibu DNA ya seli za mlango wa kizazi na kusababisha uwezekano mkubwa wa kupata kansa. Sigara pia huharibu mfumo wa kinga na hivyo kushindwa kupambana na HPV.Dawa za uzazi wa mpango-tafiti zinaonesha kuwa matumizi ya dawa za uzazi wa mpango huongeza hatari ya kupata kansa hii. Tafiti zinabainisha kuwa kwa kadri mtu anavyotumia ndivyo anavyojiweka katika hatari zaidi,kuliko anapoacha. Akiacha kutumia kwa miaka 10,hurudi katika hali ya kawaida.
Magonjwa ya zinaa-mtu mwenye magonjwa yasababishwayo na ngono kama vile kaswende na kisonono, huwa katika hatari kubwa ya kupata kansa ya kizazi.
Dalili za kansa ya mlango wa kizazi
Katika hatua za mwanzo,mgonjwa hukosa kabisa kupata dalili. Hii inakupa tahadhari kwenda kupima mara kwa mara ili kujua kama una tatizo au bado maana vinginevyo utajikuta umepata madhara zaidi. Dalili za mara kwa mara za kansa ya shingo ya kizazi ni hizi hapa;
-Kutokwa damu katikati ya hedhi
-Kutoka damu baada ya tendo la ndoa
-Kutokwa damu baada ya kukoma hedhi
-Maumivu wakati wa tendo la ndoa
-Maumivu chini ya kitovu
-Kutokwa na uchafu wenye harufu ukeni usio wa kawaida
-Hedhi yenye damu nyingi na inayochelewa kuisha
Kama kansa itakuwa imesambaa kwenye maeneo mengine ya mwili,kutokea kwenye mlango wa kizazi,mgonjwa atapata dalili zifuatazo;
-Kukojoa mkojo wenye damu
-Kukojoa mara kwa mara
-Maumivu ya mifupa
-Kuvimba kwa moja ya miguu yako
-Maumivu makali ubavuni au mgongoni yanayosababishwa na kuvimba kwa figo
-Kupoteza hamu ya kula
-Kupungua uzito
-Uchovu na kupoza nguvu
-Kukosa choo
Jinsi ya kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi
Mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia kuepuka kupatwa na saratani ya shingo ya kizazi;
Ngono salama-matatizo mengi ya kansa ya shingo ya kizazi husababishwa na maambukizi ya HPV. Ni virus wanaoambukizwa kwa njia ya ngono isiyo salama. Matumizi ya kondomu kwa kiasi fulani siyo sana yawezapunguza maambukizi. Pia hatari nyingine kubwa ni kufanya mapenzi kwa kutumia vifaa kama midoli. Lakini pia kuepuka kuanza mapenzi mapema na kutokuwa na wapenzi wengi kunaweza kukusaidia kuepuka maambukizi ya HPV
Servical screening-Hii ni njia bora ya kufanya uchunguzi wa mabadiliko ya shingo ya kizazi katika hatua za mwanzo. Wanawake wenye umri wa miaka 25-39 wanashauriwa kufanya screening kila baada ya miaka 3,wakati wanawake wenye miaka 50-64 wanashauriwa kufanya screening kila baada ya miaka 5. Hata kama una mpenzi mmoja tu,ni muhimu kufanya screening. Si mara zote majibu haya huwa sahihi,jaribu pia kumweleza daktari wako dalili ulizo nazo.
Chanjo ya HPV-Ni kweli kuwa maambukizi ya HPV ndio husababisha saratani ya shingo ya kizazi. Chanjo ya kuzuia HPV,husaidia kupunguza maambukizi ya HPV waosababisha saratani ya shingo ya kizazi.
Acha kuvuta sigara-kama tulivyoona hapo juu,uvutaji wa sigara husababisha maambukizi ya HPV,kuacha kuvuta sigara kwa upande mwingine kutakusaidia kuepuka maambukizi ya HPV na hivyo kuepuka saratani ya shingo ya kizazi.
Tiba ya saratani ya shingo ya kizazi
Tiba ya kansa hutegemea mambo yafuatayo;
-Hatua saratani ilipofikia
-Ukubwa na muonekano wa uvimbe
-Umri na afya ya mwanamke
-Hitaji la kupata mtoto baadaye
Upasuaji- upasuaji huhusisha kuondolewa kwa mfuko wa uzazi bila kuondoa ovari na mirija ya falopia.Upasuaji huu hufanyika endapo mgonjwa hatakuwa na hitaji la mtoto baadaye. Upasuaji huu wa kuondoa mfuko wa uzazi bila kuondoa ovari na mirija ya falopia unaitwa Hysterectomy.
Mionzi (radiation)- Hii hutumika kuua kansa iliyosamba sehemu zingine mbali na mlango wa kizazi. Mionzi huwa na madhara mengi kwa mgonjwa ambayo huweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu baada ya tiba ya mionzi. Madhara hayo ni kama vile;kuharisha,maumivu wakati wa kukojoa,kutokwa damu ukeni,uchovu,kichefuchefu,vidonda kwenye ngozi,uke kuwwwa mwembamba na kusababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa,ugumba,ovari na kibafu cha mkojo kuharibika.
Mchanganyo wa madawa (Chemotherapy)- Hii huweza kutumika pamoja na mionzi kuweza kuua seli za saratani.Madawa haya huchanywa na kupewa mgonjwa moja kwa moja kwenye mishipa ya damu kwa njia ya drip. Kama mionzi hapa napo kuna madhara mengi kama vile; kichefuchefu na kutapika,kuharisha,uchovu muda wote,kupungua utengenezwaji wa seli nyeupe za damu,vidonda mdomoni,kukosa hamu ya chakula na kunyonyoka nywele.
Je unasumbuliwa na kansa ya shingo ya kizazi ndugu msomaji? Wasiliana nasi kupata ushauri na tiba kupitia barua pepe maishaniafaya@gmail.com au tupigie kupitia simu 0673 923 959
Kama una maoni ama maswali kuhusiana na mada hii usisite kuwasiliana nasi kupitia kisanduku cha maoni hapo chini au tutumie barua pepe kwenye anuani hapo juu.



