Ndugu msomaji wangu leo tutatazama tatizo la vidonda vya tumbo. Miongoni mwa matatizo yaliyoshamiri na yanayosumbua sana kwa watanzania na wasio watanzania wengi ni vidonda vya tumbo. Utawasikia akina mama,akina baba,vijana wa kiume na wa kike wakilalamika mimi sili hiki au kile sababu ni vidonda vya tumbo. Wakati fulani utawaona wanajiinamia hivi wakishika tumbo kwa sababu ya maumivu au kujisikia vibaya mara tu baada ya kula,kichefu chefu na kutapika mara kwa mara na wakati mwingine kuhisi kama chakula kinataka kurudi mara baada ya kula. Sasa hivi Vidonda vya tumbo ni kitu gani, vinatokeaje,na je, inawezekana kuvidhibiti?
Vidonda Vya Tumbo Ni Nini?
Ni muhimu sana kujua vidonda vya tumbo ni nini hasa ili ujue njia bora ya kuweza kujikinga na kuepukana navyo.

Vidonda vya tumbo (Peptic Ulcers) ni vitundu
vidogo vilivyo wazi vyenye maumivu ndani ya kuta za viungo vinavyohusika na mfumo wa mmeng'enyo wa chakula. Viungo hivyo ni kama esophagus (umio),tumbo na utumbo mwembamba. Vidonda vikitokea kwenye kuta za ndani za tumbo huitwa gastric ulcers,vikiwa ndani ya sehemu ya kwanza ya utumbo mwembamba (duodenum) hivyo vinaitwa Duodenal ulcers,na vikitokea kwenye esophagus (umio) huitwa esophageal ulcers.Katika mada hii tutatumia neno vidonda vya tumbo kumaanisha aina zote za vidonda hivi.
Ugonjwa wa vidonda hutokana na hitilafu katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.
Vidonda vya tumbo hutokea pale utando unaofunika kuta za tumbo na kuzikinga dhidi ya madhara ya tindikali zilizo tumboni unapoharibiwa ama kuchubuliwa. Tindikali za tumboni (kwa mfano hydrochloric acid) husaidia kwa karibu kumeng'enya chakula. Madhara ya kuharibiwa kwa utando huu dio hupelekea ktokea kwa vidonda vya tumbo.
Chanzo Cha Vidonda Vya Tumbo
Chanzo cha kutokea vidonda vya tumbo ni kumeng'enywa kwa utando laini unaofunika tumbo.Utando huu unapochubuliwa,tindikali (hydrochloric acid) inayosaidia kumeng'enya chakula tumboni,huanza kumeng'enya kuta za tumbo moja kwa moja na kuacha michubuko (vidonda). Kuharibiwa kwa utando wa kuta za tumbo (mucosa membrane) na kusababisha vidonda vya tumbo kutokea.
Mmeng'enyo wa chakula huanza pale tu chakula kinapoingia kinywani kwa kutumia vimeng'enya (enzymes), vinavyofanya chakula kiwe rahisi kusharabiwa mwilini ili hatimaye kitumiwe na seli za mwili. Kuta za viungo vinavyohusika na mmeng'enyo wa chakula zimefunikwa na utando laini (mucosa membrane) unaosaidia chakula kupita kwa urahisi. Hitilafu kwenye mmeng'enyo wa chakula husababisha huu utando (mucus) kukwanguliwa na moja kwa moja kuta za viungo vinavyohusika na mfumo wa mmeng'enyo wa chakula huwa wazi na hivyo kuchubuliwa na tindikali (hydrochloric acid). Na hapo ndipo vidonda hutokaea.
Chanzo cha utando huu kumeng'enywa na kusababisha vidonda vya tumbo, huhusishwa na sababu nyingi,japo hizi mbili ndizo sababu mama:
.Bacteria wanaoitwa Helicobacter Pylori (H.pylori)
Bacteria hawa ndio chanzo kikubwa cha vidonda kwa walio wengi.Bacteria hawa huishi ndani yakuta za tumbo na duodenum,na huingia mwilini kupitia maji yasiyo safi na chakula. Wakati mwingine kwa njia ya mate kati ya wenzi wanaobusiana kwa ndimi.Takribani theluthi mbili ya watu wote wanaishi na bacteria hawa,japo siyo wote wamepata ugonjwa wa vidonda vya tumbo kwa sababu ya kuishi na bacteria hawa. Hawa hutengeneza enzyme inayoitwa Urease ambayo hupunguza ukali wa tindikali tumboni na kwenye duodenum. Hili likitokea tumbo ama duodenum hutengeneza tindikali kwa wingi zaidi kufidia kiwango kilichopunguzwa na hivyo kuchubua kuta za tumbo ama duodenum. Bacteria wa H pylori husababisha takribani 80% ya vidonda vya tumbo (gastric ulcers) na 95% ya vidonda ndani ya duodenum(duodenal ulcers)
.Non-steroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDs)
Hivi ni vidonge vya kutuliza maumivu kama vile maumivu ya kichwa,maumivu wakati wa hedhi na maumivu mengine madogo madogo. Vidonge hivi ni kama asprin,naproxen,diclofenac, na ibprofen.Dawa hizi hudhoofisha kuta zenye utando (mucus) za tumbo na kufanya iwe rahisi kutobolewa na tindikali.
Sababu zingine zaweza kuwa:
.Urithi-Imeonekana kuwa wagonjwa wengi wenye vidonda vya tumbo wana ndugu wengi wenye ugonjwa huo pia,hii inaonesha kuwa huu ni ugonjwa wa kurithiwa.
.Uvutaji wa sigara-Pamoja na kuwa uvutaji wa sigara huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa vidonda vya tumbo,lakini pia huongeza madhara zaidi kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo na kufanya tiba kuwa ngumu au pengine kushindikana kabisa.
.Mfumo wa maisha-Bado haijathibitishwa kuwa mfumo wa maisha kama ulaji mbaya wa vyakula,unywaji wa pombe na msongo wa mawazo husababisha vidonda vya tumbo. Lakini mfumo wa maisha huongeza athari za ugonjwa zaidi.
.Magonjwa -Baadhi ya magonjwa kama magonjwa ya ini,figo ama magonjwa ya mapafu husababisha kutokea kwa ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Dalili Za Vidonda Vya Tumbo
Dalili ya kwanza ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo ni maumivu makali ya tumbo. Maumivu hutokea kuanzia maeneo ya tumbo hadi kifuani na huwa makali wakati unapokuwa na njaa ama wakati wa usiku. Maumivu huweza kuongezeka sana wakati unapokuwa na njaa na hupungua unapokula chakula.
Dalili zingine za kuwa na vidonda vya tumbo ni kama zifuatazo:
-Matatizo wakati wa kumeza chakula
-Kujisikia vibaya baada ya kula
-Kupungua uzito
-Kukosa hamu ya kula
-Kuhisi chakula kinarudi unapokula
Lakini hali ya vidonda ikiwa mbaya zaidi dalili hizi huonekana:
-Kutapika damu
-Kupata choo nyeusi ama choo chenye damu nyeusi nyeusi
-Kichefuchefu na kutapika mara kwa mara
-Maumivu yasiyo ya kawaida kifuani na tumboni
-Kushindwa kupumua vizuri
-Joto la mwili kuongezeka hadi 38'C au zaidi
Tiba Ya Vidonda Vya Tumbo
Tiba ya vidonda vya tumbo huhusisha mambo matatu: kuondoa maumivu,kuponya vidonda na kuzuia madhara zaidi. Lakini tiba ya vidonda vya tumbo hutegemea chanzo chake. Kama chanzo ni bacteria au matumizi ya madawa ya kupunguza maumivu ama ikiwa ni mfumo wa maisha,basi unatakiwa kudhibiti chanzo ili kuwa na ufanisi katika tiba ya vidonda na kuepuka madhara zaidi. Kama utaanza tiba ya vidonda vya tumbo bila kufahamu chanzo chake na kukidhibiti basi tiba hiyo haitakuwa na ufanisi wowote. Hebu tuangalie baadhi ya tiba za vidonda vya tumbo.
.Proton pump inhibitors (PPIs)-Dawa hii huzuia kiwango cha acidi inayozalishwa tumboni. Hutolewa kwa wagonjwa ambao hawana maambukizi ya bacteria wa H pylori. Tiba yake huweza kudumu kwa muda wa miezi 2 hadi 3,lakini tatizo likiwa kubwa tiba yake huweza kudumu kwa muda mrefu zaidi. Mfano wa dawa hizo ni nexium,prevacid,prilosec,protonix,aciphex na sodium bicarbonet.
.Antibiotics-Hii hupewa mgonjwa mwenye bacteria wa H pylori. Baada ya tiba mgonjwa anatakiwa kuchunguzwa tena kujua kama H. pylori wamekufa wote. Kama itaonekana kuwepo kwa bacteria hawa baada ya tiba ya mwanzo,mgonjwa huyu anatakiwa kurudia tiba nyingine ya antibiotics. Kuna hatari japo kidogo kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo kupata kansa ya tumbo,kwa hiyo ni muhimu sana kuhakikisha unapata tiba stahiki uondokane na madhara makubwa ya baadaye. Mfano wake ni bismuth.
.H2 blockers-Hii ni dawa inayokwenda kuzuia aina fulani ya protein (histamine) ambayo huongeza utengenezwaji wa acid tumboni. Utafiti unaonesha kuw aaina hii ya protein humwagwa tumboni na kusababisha acid kutengenezwa zaidi. Mfano wa h2 blockers ni zantac,tagamet,axid na pepcids. Dawa hizi hazina uwezo wa kuwaondoa H. pylori na matumizi yake yakisimamishwa vidonda hurudia. Hizi nazo zina madhara yake kwa matumizi ya muda mrefu,mfano zantac na tagamet huweza kusababisha ugumba kwa wanaume na maziwa kuvimba kwa akina mama.
.Antacids-Hizi huyeyusha kiwango cha asidi kilicho tumboni. Mfano wa dawa hizi ni Maalox,Mylanta na Amphojel. Kazi ya kuyeyusha acid hii huwa ni ya muda mfupi na hivyo matumizi endelevu ya antacid huhitajika. Kila moja ina madhara yake,mfano maalox na Mylanta husababisha mgonjwa kuharisha na Amphojel iliyo na aluminium husababisha constipation. Matumizi ya antacids yakisimamishwa vidonda huanza tena.
.Upasuaji-Upasuaji huhitajika kama vidonda vimetoboa kuta za tumbo.
Jinsi Ya Kudhibiti Vidonda Vya Tumbo
Mambo yafuatayo ukiyafanya yaweza kukusaidia kuepuka ama kudhibiti tatizo la vidonda vya tumbo:
-Epuka matumizi ya vidonge vya kutuliza maumivu badala yake tumia maji kwa wingi
-Acha kutumia viungo vingi kwenye chakula
-Epuka kunywa pombe
-Epuka msongo kuwa na msongo wa mawazo
-Acha kuvuta sigara
-Punguza matumizi ya chai badala yake tumia mchaichai kama mbadala wako
-Epuka matumizi ya caffeine
Ndugu msomaji tumekuwa na mada ndefu juu ya tatizo la vidonda vya tumbo. Inawezekana kuwa umekuwa mhanga wa tatizo hili kwa muda mrefu na unatafuta msaada bila mafanikio. Kwa kuwa umetufahamu sasa,wasiliana nasi,utapata msaada bora na makini ili kuondokana na tatizo. Tuna dawa za kutibu tatizo hili bila madhara mengine ya ziada kujitokeza. Mada itakayofuata tutatazama Madhara Na Jinsi Ya Kuondoa Msongo Wa Mawazo. Karibu endelea kuwa nasi.
Je, unahitaji msaada kutatua tatizo la vidonda vya tumbo linalokusumbua? Wasiliana nasi kupitia barua pepe maishaniafya@gmail.com au simu 0673 923 959.



