Mzunguko wa hedhi ni mfululizo wa matukio kwa takribani siku 28 ambayo humwandaa mwanamke kwa ajili ya kutungwa mimba. Wengine huita kama mzunguko wa mwezi,wengine hutaja kitendo hiki kama kuingia mwezini. Mzunguko huu huweza kutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine. Kwa kawaida na na kwa walio wengi huchukua jumla ya siku 28 japo wapo wengine ambao huweza kwenda na kufikia siku 32. Kwa mwanamke mwenye mzunguko wa siku 28 akipata mara moja moja siku 25 hadi 30 ni jambo la kawaida kabisa. Na ili ujue mzunguko wako ni upi,hesabu siku zako zako kwa miezi sita hadi mwaka utagundua. Mzunguko wa hedhi hutokea pasipo utashi binafsi wa mtu,na ni mfululizo wa matukio unaoratibiwa na homoni zitolewazo aidha na sehemu ya ubongo (Hypothalamus na pituitary) ama ovari za mwanamke. Katika mada hii tutatazama jinsi mzunguko huu unavyotokea,Ungana nasi upate kuelewa jinsi mzunguko huu unavyotokea.
Mzunguko wa Hedhi unavyotokea
Mpangilio wote huu huratibiwa na homoni. Ziko homoni takribani nne,zinazosababisha mzunguko wa hedhi. Hebu tazama mchoro ufuatao ili uweze kuelewa jinsi mzunguko huu unavyotokea;
Huenda umekuwa ukijiuliza hedhi hutokeaje,nini kinachosababisha hedhi kutokea na ukawa unahitaji kujua jinsi hedhi inavyotokea. Hebu fuatilia kwa makini hapa upate kujua Nini hutokea hasa katika mzunguko wa hedhi.
Mwanamke kwa kawaida huzaliwa na mayai yake tayari lakini yanakuwa hauyajakomaa,na huanza kukomaa pindi tu anapovunja ungo. Anapofikia umri wa miaka 14 kwa walio wengi (wengine huanza miaka 11) mayai yake hukomaa na kuwa rahisi kwake kupata mimba. Hapa mwili wako hujianda kila mwezi kwa ajili ya kushika mimba. Yai moja huachiwa toka katika ovari na kuingia katika mirija ya falopia ili lirutubishwe na mwanamke ashike mimba. Kama yai lililoachiwa halitarubishwa,ile ngozi nyororo iliyoandaliwa kupokea yai lililorutubishwa ndani ya mfuko wa uzazi,hunyofoka na kutoka nje na kitendo hiki huitwa menstruation.
Mzunguko wa Hedhi unaweza kugawanywa katika hatua tatu kama ifuatavyo;
Follicular phase
Ovulation phase
Luteal phase
1. FOLLICULAR PHASE
Mwanamke anapovunja ungo,tezi ya Hypothalamus inayopatikana katika ubongo huanza kutengeneza homoni inayoitwa Gonadotrofin Releasing Hormone (GnRH). Homoni hii husafirishwa hadi katika sehemu ya juu ya tezi ya Pituitary (anterior pituitary). Ndani ya pituitary Gonadotrofin Releasing Hormone (GnRH) husababisha pituitary itengeneze homoni mbili muhimu ambazo ni Follicle stimulating hormone na Lutenizing Hormone.
Follicle stimulating hormone (FSH) huamsha ovari ili zianze kufanya kazi.Ndani ya ovari FSH husababisha kukuzwa kwa mayai ndani ya vifuko vya mayai vinavyoitwa follicles. Kwa kadri mayai yanavyokuwa,follicle hizi pia hukua na kukomaa. Follicle zinapokomaa huzalisha homoni mbili yaani oestrogen na testesterone.
Katika kipindi cha siku 7 hadi 10 kiwango cha oestrogen huendelea kuongezeka. Kwa kipindi hiki mwanamke hujisikia mtulivu ,mwenye furaha na anayependa kutoka na kuwa vizuri muda wote. Ni katika kipindi hiki mwanamke huweza kufanya maamuzi yenye busara na kujiamini na kufikiria ama kuweza kutekeleza mipango mikubwa. Ni kipindi ambacho mwanamke huwa na uwezo mkubwa wa kuthubutu. Homoni ya testesterone kwa upande mwingine humfanya mwanamke kuwa na hamu kubwa ya kufanya mapenzi,na kama yuko karibu na mwandani wake hujisikia vizuri kuwa naye karibu na kufurahi. Baada ya siku kumi kiwango cha oestrogen huongezeka na kusababisha kuongezeka pia kwa kiwango cha LH inayozalishwa ndani ya pituitary. Kuongezeka huku kwa kiwango cha oestogen hupunguza kiwango cha FSH. Leutenizing Hormone itakapoongezeka sana husababisha follicle iliyokomaa kupasuka na kuachia yai kitendo kinachitwa ovulation.
Kabla hatujaangalia ovulation phase,hebu tuangalie kidogo kazi za oestrogen hormone;
-Oesrogen ikiwa katika kiwango kidogo huzuia kuzalishwa kwa Leutenizing Hormone (LH) toka ndani ya tezi ya pituitari.
-Katika kiwango kidogo huongeza kuzalishwa kwa FSH ili kukomaza follicle kabla ya ovulation
-Katika kiwango kikubwa Oetrogen husababisha kutengenezwa kwa wingi kwa LH ili kusababisha ovulation
Katika kiwango kikubwa Oestrogen huzuia kutengenezwa kwa FSH ili kuzifanya follicle ziasuke na kiachia yai.
-Husababisha mifupa na misuli kukua
-Husababisha kutengenezwa kwa kuta laini za mfuko wa uzazi (uterus) yaani (Endometrium linning).
-Hudumisha tabia za kike
Basi sasa hebu tuangalie sehemu ya pili ya yai kutolewa-Ovulation.
2. OVULATION PHASE
Baada ya ovulation,kiwango cha Luteinizing hormone (LH) na Gonadotrofin releasing hormone (GnRH) hupungua kama inavyoonekana kwenye mchoro hapo juu. Follicle zikishapasuka na kutoa yai hufa. Follicle hizi sasa huitwa Corpus Luteum.
3.LUTEAL PHASE
Hii hatua inaitwa hivyo kwa sababu ya corpus luteum. Corpus Luteum ni neno linaloamanisha kitu chenye rangi ya njano kwa lugha ya kilatini. Corpus Luteum ni mabaki ya follicle baada ya ovulation kukamilika.
Corpus luteum hutengeneza homoni mbili;
-Progesterone
-Inhbin
Inhibin huenda moja kwa moja na kuzuia utengenezwaji wa Follicle stimulating hormone (FSH) toka ndani ya tezi ya pituitari.
Progesterone huimarisha kuta za uterus ili yai lililorutubishwa liweze kujishikiza. Hii ndio homoni inayoimarisha kuta za mfuko wa mimba wakati wote mama anapokuwa mjamzito. Kama haitatengenezwa kwa kiwango cha kutosha, mimba hiyo huwa katika hatari ya kutoka maana kuta za uterus huwa dhaifu kiasi cha kuachia na kuchanika kabisa.
Corpus luteum huweza kudumu kwa siku 12 hadi 14. Muda wa kudumu kwa corpus hautofautiani kati ya mwanamke mmoja na mwingine kama ilivyo kwenye follicular phase ambapo kunaweza kuwa na utofauti kwa mwanamke mmoja na mwingine.
Kama yai halitarutubishwa corpus luteum inakufa na kiwango cha progesterone na oestrogen mwilini hupungua kabisa. Kupungua kwa Progesterone husababisha kuta za uterus kuanza kuchanika. Kuta hizi zitakapochanika hutoka nje ya mwili wa mwanamke kitendo hiki ndicho kinachoitwa menstruation (hedhi).
Siku Bora Za Kupata Mtoto
Kuna baadhi ya wanawake wamekuwa wakilalamika kukosa watoto kwa muda mrefu wakati mwingine ni kutokana na kukosea kuhesabu siku zao. Simaanishi kukosea siku ni sababu za ugumba kwa mwanamke,bali kukosa kupata watoto kwa sababu ya uzembe.
Ili kujua ni siku gani bora ya kupata mtoto ni lazima kwanza utambue mzunguko wako ni wa siku ngapi. Ili kujua mzunguko wako hesabu idadi ya siku kuanzia siku ya kwanza kuona damu hadi siku moja kabla hujaona damu tena. Idadi ya siku hizo ndizo siku za mzunguko wako.
Angalia kielelezo kilichoko hapa chini kuonesha mzunguko wa siku 28. Ukihesabu kuanzia day one,utaona kabla ya day one nyingine (siku ya kuona damu) zitakuwa zimepita siku 28.
Siku bora za mwanamke kupata mtoto ni siku za yai kutolewa (ovulation days). Kwa kawaida yai hutolewa siku ya 14 kabla ya mzunguko mwingine kuanza. Hii hutegemea mzunguko wako ni wa siku ngapi. Kama mzunguko wako ni siku 28 uwezekano wa yai kutoka ni siku ya 14 baada ya mzunguko wa pili kuanza na ikiwa mzunguko wako ni wa siku 30 yai laweza kutoka siku ya 16 baada ya mzunguko kuisha.
Kwa kila mzunguko huwa na siku 6 za mwanamke kuweza kupata mimba. Siku hizo ni siku ya 11 hadi siku ya 16 baada ya mzunguko kuanza. Siku za mwanamke kuweza kupata mimba huitwa siku za hatari kwa kila mzunguko. Siku za hatari ni kati ya siku 3 kabla ya siku ambayo yai hutolewa na siku 2 baada ya yai kutolewa. Kwa mfano mwanamke mwenye mzunguko wa siku 28,siku za hatari kwake.
Angalia kielelezo kifuatacho kuelewa siku bora ya kupata mimba;
Katika moja ya siku hizo,mwanamke akifanya tendo la ndoa na mwenzi wake ni rahisi sana kupata mimba. Hii ni kwa sababu yai la mwanamke litakalotolewa siku ya 14 (kwa mwanamke mwenye mzunguko wa siku 28) lina uwezo wa kuishi kwa masaa 12 hadi 24 na mbegu za mwanamume zinaweza kuishi kwa siku 3 hadi 5 baada ya kutolewa.
Kwa hiyo mwanamke akishiriki na mwanamume siku yoyote kati ya hizo sita kama tulivyoona hapo juu,ataweza kupata mimba kama tu mbegu za kiume zitakuwa zimekomaa. Kwa mfano kama ni siku ya 11 mbegu zitabaki hai hadi siku yai linatolewa na hivyo zaweza kulirutubisha. Lakini hata kama ingekuwa siku ya 14 au 15 ni rahisi kwa sababu yai litakuwa na siku nzima ya kuwa hai na hivyo litaweza kurutubishwa.
Naamini umeelewa vema ndugu msomaji na sasa unaweza kupanga kama unataka mtoto sasa,kazi yako ni kulengesha tu katika moja ya siku za hatari. Leo tutaishia hapo kwa kuwa mada hii ni ndefu. Endelea kuungana nasi katika mada zitakazofuata tutakapotazama maumivu kabla ya hedhi na maumivu wakati wa hedhi kama inavyoweza kutokea kwa baadhi ya watu kuumwa wakati hedhi ikiendelea.
Tafadhali usiache kutoa maoni,ushauri ama kuuliza maswali yako kuhusiana na mada hii.Tuandikie kupitia maishaniafya@gmail.com ama simu 0673 923 959.





