Kusongwa na mawazo si jambo baya kabisa. Kwa namna fulani mawazo ama kufikiria sana hukupatia msukumo na hamasa ya kufikia ama kutekeleza kile kinachokusumbua mara kwa mara. Kusongwa na mawazo humpatia mtu namna bora yakufanikisha mipango na mikakati aliyo nayo. Hata hivyo pale msongo wa mawazo unapoathiri afya yako kiakili,kimwili na kihisia,huo ni msongo mbaya wa mawazo. Katika mada hii tutatazama madhara ya msongo wa mawazo.
Inawezekana unadhani kuwa ni vigumu kukabiliana na msongo wako,hapana kuna njia bora za kuukabili msongo. Kuna watu wengine hutumia njia mbovu za kukabili msongo kama vile kunywa pombe,kutumia madawa ya kulevya,kuvuta sigara,kukaa kwenye TV au kompyuta kwa muda mrefu,kutumia vidonge,kujitenga na jamii,kulala sana,kugombana na kupigana. Hebu ungana nami katika mada hii upate kujua jinsi unavyopaswa kukabiliana na msongo wako wa mawazo kama unakabiliwa na athari zake sasa.
Inawezekana unadhani kuwa ni vigumu kukabiliana na msongo wako,hapana kuna njia bora za kuukabili msongo. Kuna watu wengine hutumia njia mbovu za kukabili msongo kama vile kunywa pombe,kutumia madawa ya kulevya,kuvuta sigara,kukaa kwenye TV au kompyuta kwa muda mrefu,kutumia vidonge,kujitenga na jamii,kulala sana,kugombana na kupigana. Hebu ungana nami katika mada hii upate kujua jinsi unavyopaswa kukabiliana na msongo wako wa mawazo kama unakabiliwa na athari zake sasa.
Chanzo cha msongo wa mawazo
Jambo lolote laweza kusababisha msongo. Lakini si kila jambo lisababishalo msongo kwako litamsababishia na mwingine. Sababu za msongo wa mawazo huweza kuwa changamoto mbaya za kimaisha kama vile kufukuzwa kazi, ama hali za furaha maishani kama vile kuoa au kupata mtoto. Kwa watu wengine kufikiria jambo sana huweza kusababisha msongo kwao.
Mwili wako una namna ya moja kwa moja ya kujihami. Unapopatwa na mshituko au hatari ya namna yoyote,mwili wako huzalisha kemikali za kukusaidia kukabili changamoto au kukupa uoga ukimbie hatari hiyo. Tendo hili huratibiwa na mfumo wa neva za fahamu,unaotawala matendo yasiyo ya hiari.
Mwili wako huzalisha homoni za cortisol,adrenaline na noradrenaline ambazo huuandaa mwili kwa ajili tendo la ghafla lililoupata mwili. Homoni hizi husababisha mapigo ya moyo kuongezeka,misuli hukaza,mgandamizo wa damu (blood pressure) huongezeka,mtu kupumua haraka haraka na pia huongeza uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi haraka. Mabadiliko haya yakitokea huuandaa mwili kuabiliana na lolote lililojitokea. Hebu sasa tuangalie baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha mtu kukabiliwa na msongo wa mawazo.
.Kuachwa na mke au mme
.Kufungwa jela
.Kufiwa na ndugu wa karibu
.Kupatwa na ajali au ugonjwa
.Kuoa au Kuolewa
.Kufukuzwa kazi
.Kustaafu kazi
.Matatizo ya kifamilia
.Kukosa pesa
.Migogoro kazini
.Kupata ujauzito
.Mimba kuharibika
.Kutoa mimba
.Kelele nyingi
.Kuwa na majukumu mengi
Dalili za msongo wa mawazo
Msongo ukidumu kwa muda mrefu matatizo kadha wa kadha ya kiafya huweza kujitokeza. Msongo huweza kuwa endelevu pale chanzo chake kitakapodumu kuwa kilekile. Watu hupata dalili za msongo wa mawazo kwa namna mbalimbali. Wengine hupatwa na tatizo la chakula kushindwa kumeng'enywa vyema,wengine maumivu ya kichwa,wengine huzuni na nyinginezo nyingi. Watu wenye msongo wa kudumu kwa muda mrefu hupatwa na maambukizi ya mafua yasiyokwisha. Hebu tutazame dalili hizi;
.kusahau
.Kuchoka
.Kukosa usingizi
.Kichwa kuuma
.Kukosa uwezo wa kufikiri vyema
.Kukakamaa kwa misuli ya shingo
.Tumbo kuuma
.Hofu
.Kukosa kujiamini
.Kukosa utulivu
.Kushindwa kufanya maamuzi sahihi
.Kushindwa kula au kula sana
Mambo yanayoongeza uwezo wa kudhibiti msongo wako
Kuukabili msongo huweza kuwa changamoto kwa walio wengi. Kuna watu hufanikiwa kumudu magumu ya msongo kwa sababu ya maandalizi au ujasiri wa kukabili mambo haijalishi ukubwa au ugumu wake bila kuathirika kwa kiwango kikubwa. Mambo yafuatayo yaweza kumsaidia mtu yeyote kukabili msongo wa mawazo;
Mtandao wako wa msaada-kuwa na mtandao wa watu walio karibu nawe kama marafiki ama ndugu,hukupunguzia hatari ya kukabiliwa na msongo. Kama una watu sahihi wa kushirikiana nao,changamoto za maisha hazitakukosesha usingizi. Kwa upande mwingine,kukosa watu wa karibu kutakuweka katika hatari kubwa ya kushindwa kuukabili msongo.
Mtazamo wako-mtazamo wako juu ya maisha na changamoto zake zisizozuilika huathiri uwezo wako kukabiliana na msongo. Kama wewe ni mwenye matumaini na mwenye kujiamini,unaweza kuathiriwa na msongo kwa kiwango kidogo sana. Watu jasiri hupokea changamoto,wana hisia imara,wanaamini katika mikakati mikubwa na hupokea mabadiliko kama vitu visivyoepukika maishani. Hawa huweza kukabili msongo bila kuathirika.
Uwezo wa kutawala hisia zako-kama hutajua jinsi ya kujituliza unapokuwa na huzuni,hasira au hofu,una hatari kubwa ya kuathiriwa na msongo. Ukiweza kutawala hisia zako,utaongeza uwezo wako wa kuumudu msongo wa mawazo.
Uelewa wako na maandalizi-ukiwa na uelewa juu ya jambo linalosababisha msongo na kwamba litakwisha lini,itakuwa rahisi kwako kuukabili msongo.Ukilijua jambo mapema ni rahisi kwako kujiandaa na hali hiyo kabla haijafika.
Madhara ya msongo wa mawazo
Msongo huweza kuathiri fikra,hisia,tabia na mwili kwa ujumla. Hebu tutazame athari za msongo hapa;
Athari za Msongo Kimwili
-Maumivu ya kifua
-Kuwa na kawaida ya kutoa jasho sana
-Magonjwa ya moyo
-Kuumwa kichwa
-Matatizo ya misuli
-Watoto kupata unene kupita kiasi
-Kinga dhidi ya magonjwa kupungua
-Kukosa usingizi
-Maumivu ya tumbo
Athari za Msongo Kiakili na kihisia
-Hasira
-Hofu
-Mfadhaiko
-Hisia za kukosa ulinzi
-Kusahau
-Mshituko
-Uchovu
-Kukosa utulivu
-Huzuni
Madhara ya Msongo kitabia
-Kula sana
-Kula kidogo sana
-Kubagua chakula
-Hasira
-Kunywa pombe
-Kutumia sigara sana
-Kutumia madawa ya kulevya
-Kujitenga na jamii
-Kulialia
-Kutoelewana na jamii
Njia za kuondoa Msongo wa Mawazo
Fanya mazoezi-Mazoezi si kwamba yanaondoa msongo wako,bali yanapunguza mzigo wa hisia unaokuelemea na kukufanya ushughulike na mawazo yako kwa utulivu.
Jumuika na wengine-kitendo cha kuongea na wengine uso kwa uso huweza kuamsha homoni inayoondoa msongo unapokuwa hijisikii amani kabisa. Tumia muda wako na watu watakaokufanya ujisikie vizuri na usiruhusu majukumu yako kukutenga na maisha ya kijamii. Kama huna watu wa kushirikiana nao,hutakuwa na mahali pa kukimbilia utakapokuwa unahitaji msaada.Mambo tunayofanya na jamii hutufanya tufarijike. Tukiwa na marafiki tutacheka pamoja,kitendo kinachosaidia kuondoa msongo kwa haraka.Kufanya mambo na marafiki hukuwezesha kupata suluhisho kwa haraka.
Pumzika-unaweza usifanikiwe kuondoa msongo wote,lakini unaweza kupunguza madhara yake kwako. Kupumzika kutapunguza mawazo mengi na kuuweka mwili wako katika hali ya furaha na utulivu.
Epuka mazoea mabaya-kuna watu hudhani kunywa pombe,kuvuta sigara au kutumia madawa ya kulevya ni suluhisho la tatizo la msongo! Kwa kufanya hivi hupunguzi tatizo bali unaongeza tatizo. Matumizi ya vitu hivi yaweza tu kukusahaulisha kidogo lakini baada ya hapo hali huanza tena na huenda ikawa mbaya kuliko kawaida. Kwa hiyo unashauriwa kutafuta mbinu bora za kuondoa msongo sio za ulevi.
Kuwa na mtazamo chanya-mara nyingi msongo hutokana na kutazama upande hasi wa jambo. Jaribu kutazama upande chanya sasa. Tazama upande uliofanya vizuri. Hata kama glass ina maji nusu tu,usitazame sehemu isiyo na maji tu bali tazama sehemu yenye maji itakufariji sana. Jipongeze katika mambo uliofanya vizuri na kisha jipe amani.
Kubaliana na mambo yaliyo nje ya uwezo wako-kubadili mambo magumu ni vigumu. Jaribu kushughulika na mambo unayoyamudu tu. Kuhangaika na mambo yaliyo nje ya uwezo wako ni sawa na kusukuma ukuta usioweza kusogea,hali itakayosababisha msongo wako kuwa mkubwa zaidi.
Jitulize mwenyewe-kila tatizo lina suluhisho lake. Kama utakaa na kusema siwezi fanya lolote kwa tatizo langu hili,hali yako itakuwa mbaya kuliko kawaida. Hisia za kutojiamini kwa zenyewe ni chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo kuongezeka. Kujiamini na kujituliza ni hatua muhimu ya kutatua tatizo na kukuletea ufanisi wewe peke yako na si mwingine.
Wasaidie wengine-tafiti zinaonesha kuwa kuwasaidia wengine walio na hali mbaya kuliko ya kwako,huyafanya matatizo yako
yaonekane kuwezekana. Kwa kadri unavyosaidia ndivyo unavyojisikia furaha na amani.
Kula chakula chenye afya-chakula unachokula kinaweza kujenga au kubomoa uwezo wako wa kukabiliana na changamoto. Vyakula vya sukari,nafaka zilizokobolewa ama vilivyosindikwa huongeza ubaya wa tatizo lako,lakini ulaji wa matunda,protein,mafuta yanayotakiwa (omega-3) na mboga za majani husaidia mwili kukabiliana na mikikimiki ya maisha.
Pata usingizi mzuri-lala angalau kwa 7 hadi 8 ili kuweka mwili wako katika hali nzuri ya utulivu.
Tafuta msaada wa karibu kwa watu sahihi-waambie watu wako wa karibu,ndugu na marafiki kuhusu matatizo yako,kama unaamini ni watu sahihi na wanaweza kukupa msaada. Ni muhimu kujua unamwambia nani,maana kama hujawa makini ukamshirikisha mtu asiye sahihi utaongeza matatizo na siyo suluhisho.
Ndugu msomaji je, una tatizo la msongo wa mawazo,na ungependa kupata msaada? Unaweza kupata suluhisho kwetu. Wasiliana nasi, 0673 923 959
Vipi mada hii imekuwa na msaada wowote kwako? Kama ndivyo,usisahau kutoa maoni ama kuuliza swali kuhusiana na mada hii. Kwa msaada,maswali,maoni ama ushauri kuhusu mada hii, Tafadhali usisite kutuandikia kupitia maishaniafya@gmail.com ama piga simu 0673 923 959.





